UCHAGUZI SERIKALI ZA MITAA NOV. 27, 2024 HATUKUPATA TAARIFA ZA RUSHWA – TAKUKURU MKOANI PWANI
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Pwani,umebainisha kwamba uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji ambao umefanyika Nov 27, mwaka huu, taarifa za matukio yanayohusisha vitendo vya rushwa kwa wagombea na wadau wengine wa uchaguzi hazikupatikana.
Mkuu wa Takukuru mkoani Pwani Kamanda, Christopher Myava, akizungumza na Waandishi wa Habari mkoani humo, leo Desemba 5, 2024 amesema sababu kubwa ya vitendo vya rushwa kutopatikana katika uchaguzi huo imetokana na wananchi, wagombea, wasimamizi na viongozi wa vyama vya siasa kuwa na uelewa wa kutosha kuhusu athari za rushwa.
“Kabla ya uchaguzi tulikuwa tukitoa elimu mara kwa mara kwa viongozi, wagombea, wasimamizi na wananchi lengo likiwa wasijihusishe na vitendo vya rushwa, hivyo tunaweza kusema kwamba uchaguzi huo katika Mkoa wa Pwani umekwenda vizuri na kwetu ni mafanikio makubwa.
“Ni imani yetu kwamba elimu ya mapambano dhidi ya rushwa tunayoendelea kuitoa itasaidia siku zijazo kuwa na chaguzi ambazo zinafanyika bila kuwepo viashiria vya vitendo vya rushwa jambo litakalosaidia kupata viongozi makini wanaoingia madarakani bila kutoa rushwa,” amesema.
Kamanda Myava, ameongeza kuwa licha ya kutoa elimu wakati wa mchakato wa maandalizi ya uchaguzi huo, pia wakati wa upigaji kura walijipanga vizuri na kutembelea vituo mbalimbali vya upigaji kura mkoani humo na hawakubaini uwepo wa rushwa na kufanya uchaguzi huo kwenda vizuri.
Pia amesema wanaendelea kujipanga vema na kutoa elimu ya mapambano ya rushwa kwa makundi mbalimbali ili Uchaguzi Mkuu ujao ufanyike bila kuwepo vitendo vya rushwa mkoani humo.
“Nawaomba wananchi waendelee kushirikiana nasi kwa kutoa taarifa za rushwa kwetu ili tuzifuatilie na kuzifanyia uchunguzi wa kutosha na watakabainika tutawachukulia hatua stahiki kwa kuwafikisha mahakamani.
“Ukiachana na uchaguzi kwenye maeneo yao kuna miradi ya maendeleo inafanyika wakibaini tu kuna mianya ya rushwa watujulishe kupitia namba ya bure 113 na namba ya Kamada Takukuru Mkoa wa Pwani ni 0738150176,” amesema.
Comments
Post a Comment