KAMATI YA UONGOZI WA MRADI WA JNHPP YAKAGUA MAENDELEO YA BWAWA LA JULIUS NYERERE
Kamati ya Uongozi wa Mradi wa Bwawa la Julius Nyerere (JNHPP), tarehe 26 Februari 2026, imekagua maendeleo ya uzalishaji wa umeme katika mradi huo na kueleza kuridhishwa na usimamizi pamoja na utekelezaji wake, uliokidhi viwango vya ubora vinavyoendana na thamani ya fedha iliyowekezwa na Serikali. Mwenyekiti wa Kamati hiyo, ambaye pia ni Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Dkt. Jim Yonazi , amesema kamati imefurahishwa na namna bwawa hilo linavyochochea ukuaji wa uchumi kwa kuongeza uzalishaji wa umeme unaosambazwa katika maeneo mbalimbali nchini, hatua inayochangia kuimarika kwa upatikanaji wa nishati ya umeme. “Tumeridhishwa na jinsi mradi huu ulivyosimamiwa na kutekelezwa kwa ufanisi mkubwa. Ukilinganisha na miradi mingine barani Afrika, mradi huu umejengwa kwa ubora wa hali ya juu na umeleta unafuu katika huduma ya umeme nchini. Haya ni mafanikio makubwa kwa Taifa,” alieleza Dkt. Yonazi. Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishat...