Skip to main content

SERIKALI MBIONI KUFUTA LESENI ZA MADINI ZINAZOKIUKA MASHARTI


Serikali kupitia Wizara ya Madini imetoa hati za Makosa kwa Kampuni 95 yaliyopewa leseni za Uchimbaji Mkubwa na wa Kati wa Madini kutokana na wamiliki wa leseni hizo kukiuka masharti ya Leseni kama yalivyoainishwa kwenye Sheria ya Madini.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Mei 6, 2025 jijiini Dar es Salaam, Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde amesema kuwa msimamo thabiti wa serikali ni kwamba kampuni ambayo imepewa leseni ya uchimbaji tumewaandikia hati za makosa na ndani ya siku 30 waeleze sababu kwa nini wasifutiwe leseni hizo.

Mh. Mavunde ameeleza kuwa hati hizo za makosa zimetolewa rasmi kuanzia Aprili 14, 2025 na muda wake utamalizika Mei 13 mwaka huu. 

 “Kama wanahoja walete majibu yao, tuyahakiki tukijiridhisha na hoja zao tutawaondolea makatazo kama hawana hoja tutawafutia leseni zao kwa mujibu wa Sheria ya Madini Sura 123 ya utoaji na ufutaji wa leseni za madini na uchimbaji kifungu cha 63 na Kanuni zake, ambacho kinaeleza ukipewa leseni unapaswa uanze kazi ndani ya miezi 18.

Amesema, Serikali imetoa leseni kwa wachimbaji wa kati na wakubwa ambazo tangu kutolewa kwake hazifanyiwa kazi.

Zipo Kampuni tangu zimechukua leseni mwaka 2011 mpaka leo hazijaingiza hata koleo kwenye eneo miaka 14 sasa hazijaanza shughuli zozote, hatuwezi kuwa nchi ya namna hii.

Leseni 7 tu kati ya 95 ukiziweka pembeni zina mtaji wa Shilingi Trilioni 15 zimelala, sisi hatuwezi kuwa nchi ambayo inatoa leseni kwa ajili ya kuchochea sekta ya madini kukua,halafu kuna watu wanachukua leseni wanakaa nazo hawafanyii kazi kwa kisingizio kuwa tupo kwenye mazungumzo na serikali na sababu mbali mbali.

Leseni za madini zikitolewa zina masharti nyuma yake kwenye ile karatasi hakuna sharti linalosema mtu ataanza uchimbaji wa madini nchini Tanzania akikamilisha mazungumzo na serikali, hiyo si sehemu ya sharti.

Masharti ni kwamba mwombaji anapopewa leseni ni lazima aanze uchimbaji ndani ya miezi 18 vinginevyo awe na sababu ambazo zimeridhiwa na Waziri wa Madini kupitia Tume ya Madini, vinginevyo unapaswa kuanza uchimbaji ndani ya miezi 18.

Amesema na wale wote ambao wamepata hati ya makosa ambao wamejibu waende na barua ya ‘Commitment’ ya kueleza wataanza uchimbaji lini, ambao katika barua hiyo pia ikitokea ameshindwa kukidhi kile alichosema kwenye barua sheria itafuata mkondo wake.

Sekta ya Madini ni kati ya sekta zenye mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa nchi hivyo shughuli za uchimbaji wa madini huchochea maendeleo makubwa ya kiuchumi


Comments

Popular posts from this blog

SEKTA YA NISHATI IWE KICHOCHEO CHA KUIUNGANISHA AFRIKA KUJENGA UCHUMI