SEKTA YA MICHEZO YAIMARIKA KWA KASI
Sekta ya sanaa na michezo imeimarika kwa kasi katika kipindi cha uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Kwa mfano Mirabaha kwa wasanii waliosajiliwa na COSOTA imeongezeka kutoka shilingi milioni 245 mwaka 2020 hadi shilingi milioni 687.7 mwaka 2024, hatua iliyoongeza kipato na hadhi na tija kwa wasanii.
Kupitia Mfuko wa Utamaduni na Sanaa, mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 5.35 imetolewa kwa miradi 359 mwaka 2025, ikilinganishwa na shilingi bilioni 2.69 kwa miradi 143 mwaka 2021.
Katika hatua nyingine sekta hii imechangia kwa kiasi kikubwa katika kuongeza ajira, ambapo idadi ya walioajiriwa imeongezeka kutoka 286,985 mwaka 2021 hadi 449,531 mwaka 2024. Mbali na mafanikio haya kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi yetu, Tanzania imefanikiwa kupata heshima kubwa ya kuwa mwenyeji wa mashindano ya CHAN mwaka 2025 na AFCON mwaka 2027.
Ndio maana ndani ya kipindi kifupi ujenzi wa miundombinu ya viwanja umetekelezwa kama vile ujenzi wa uwanja mpya wa kisasa wa mpira wa miguu unaojulikana kama Samia Suluhu Stadium jijini Arusha unaendelea kwa gharama ya shilingi bilioni 298.
Sekta hii ni miongoni mwa sekta zinazokua kwa kasi kubwa , ikiongoza kwa wastani wa asilimia 17, na kutoa mchango mkubwa kwa uchumi pamoja na kuimarisha hadhi ya Tanzania katika medani za kimataifa.


Comments
Post a Comment