DKT. BAKARI - ANWANI ZA MAKAZI NI MSINGI MUHIMU UKUAJI UCHUMI WA KIDIJITALI

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Dk. Jabir Bakari, amesema kuwa uwepo wa anwani za makazi zilizoandaliwa vizuri ni msingi muhimu wa kukuza uchumi wa kidijitali, kwani huwezesha huduma mbalimbali kuwafikia wananchi kwa haraka na kwa ufanisi zaidi.

Dk. Bakari ameyasema hayo leo Februari 5, 2026 jijini Dar es Salaam alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari wakati wa Kongamano la Mwaka la Anwani za Makazi na Maonyesho ya Teknolojia ya Huduma za Posta. Amesisitiza kuwa matumizi sahihi ya anwani za makazi humsaidia mwananchi kutambulika anapoishi na kurahisisha upatikanaji wa huduma na bidhaa mbalimbali.

Ameeleza kuwa, “Kuwa na anwani za makazi ni jambo la msingi sana, kwani bila anwani huwezi kuwa na uchumi wa kidijitali unaofanya kazi ipasavyo. Ni muhimu kuhakikisha maeneo mapya na yanayofanyiwa maboresho yanapewa anwani sahihi za makazi ili mfumo huu uweze kufanya kazi kikamilifu.”

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Masoko na Mauzo wa Shirika la Posta Tanzania, Fredinand Kabyemela, amesema kuwa utoaji wa huduma za posta hauwezi kufanyika kwa ufanisi bila uwepo wa anwani za makazi.

Kabyemela amesema Shirika la Posta linaendelea kuwahamasisha wananchi kuwa mstari wa mbele katika kutunza miundombinu ya anwani za makazi, ili kuwezesha utoaji wa huduma muhimu kama usalama, afya na elimu kwa urahisi zaidi.

Wiki ya Anwani za Makazi inatarajiwa kuhitimishwa Februari 8, 2026, ikiwa na lengo la kuwahamasisha wananchi kujisajili na kutumia anwani za makazi ili kurahisisha biashara na huduma mbalimbali katika uchumi wa kidijitali.






Comments

Popular posts from this blog

SEKTA YA NISHATI IWE KICHOCHEO CHA KUIUNGANISHA AFRIKA KUJENGA UCHUMI