BEI YA UFUTA YAFIKIA SHILINGI 2,520 KWA KILO KATIKA MNADA WA KWANZA TAMCU TUNDURU
Chama Kikuu cha Ushirika wa Mazao Wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma (TAMCU) kimefanya mnada wa kwanza wa zao la ufuta kwa msimu wa 2026/2027 kupitia mfumo wa kidijitali wa TMX.
Mnada huo umefanyika tarehee 21/5/2026 katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, ambapo bei ya juu ilikuwa Shilingi 2,520 kwa kilo na bei ya chini ikiwa Shilingi 2,410 kwa kilo, huku wastani wa bei ukiwa Shilingi 2,477 kwa kilo. Wakulima walioshiriki mnada huo wamekubali kuuza zao lao kwa bei hiyo.
Akizungumza na wakulima baada ya kutangaza matokeo ya mnada huo, Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Denis Masanja, amewataka wanunuzi kuhakikisha wanalipa fedha kwa wakati ili wakulima waliouza zao hilo waweze kupata malipo yao mapema na kuendelea na shughuli zao za kiuchumi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika Tunduru TAMCU, Mussa Manjaule, amesema bei hiyo inaridhisha ikilinganishwa na bei ya msimu uliopita. Aidha, amemhakikishia Mkuu wa Wilaya kuwa hata kama wanunuzi watachelewa kulipa, TAMCU iko tayari kuhakikisha wakulima wanapata fedha zao kwa wakati, kama ilivyokuwa katika misimu mingine.
Katika mnada huo wa kwanza, jumla ya kilo 994,618 za ufuta zimeuzwa. Aidha, mnada wa pili unatarajiwa kufanyika tarehe 26/05/2026 katika Tarafa ya Lukumbule kupitia Chama cha Msingi cha Nguvumali AMCOS.






Comments
Post a Comment