DC NDILE AWATAKA VIJANA KUFANYA KAZI KWA BIDII

 


Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) umetoa elimu kwa zaidi ya vijana 300 wa Halmashauri ya Wilaya ya Madaba kuhusu fursa mbalimbali za kiuchumi zinazopatikana kupitia rasilimali za misitu, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuwawezesha vijana kujikwamua kiuchumi kupitia sekta ya misitu.


Elimu hiyo imetolewa katika jukwaa la vijana lililofunguliwa rasmi na Mkuu wa Wilaya ya Songea Kapenjam Ndile ambaye amewataka vijana kuzingatia maadili mema, nidhamu na uwajibikaji ili waweze kutumia vyema fursa zinazotolewa na Serikali pamoja na taasisi mbalimbali.


Akizungumza katika jukwaa hilo, Mheshimiwa Ndile amesema mafanikio ya vijana yanategemea juhudi binafsi, uaminifu na kujituma katika kazi, huku akibainisha kuwa changamoto kubwa kwa vijana wengi si ukosefu wa fursa bali ni ukosefu wa nidhamu na uwajibikaji.


Katika mada iliyowasilishwa na Mhifadhi Daraja la kwanza (CR1) Daud Mandingo kwa niaba ya Mhifadhi Mkuu wa TFS Shamba la Miti Wino, vijana walielimishwa kuhusu fursa zinazopatikana kupitia shughuli mbalimbali za misitu ikiwemo ajira za msimu katika Shamba la Miti Wino, hususan shughuli za palizi na utunzaji wa mashamba ya miti.


Aidha, Mhifadhi Mandingo alibainisha fursa nyingine zinazotolewa na TFS kuwa ni pamoja na ufugaji wa nyuki, ugawaji wa miche ya miti, elimu ya upandaji na uhifadhi wa misitu pamoja na ugawaji wa mizinga kwa vikundi vya vijana kwa lengo la kuwawezesha kujiajiri na kuongeza kipato.


Wakieleza mtazamo wao, baadhi ya vijana walioshiriki jukwaa hilo wamesema elimu waliyoipata imewasaidia kutambua fursa zilizopo katika sekta ya misitu na kuwaongezea hamasa ya kushiriki katika shughuli za uzalishaji na uhifadhi wa mazingira.






Comments

Popular posts from this blog

SEKTA YA NISHATI IWE KICHOCHEO CHA KUIUNGANISHA AFRIKA KUJENGA UCHUMI