MBINGA DC YAVUKA LENGO LA MAKUSANYO, YAFIKIA BILIONI 12.1 KABLA YA MWISHO WA MWAKA WA FEDHA
Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga iliyopo mkoani Ruvuma imefanikiwa kuvuka lengo la ukusanyaji wa mapato katika mwaka wa fedha 2025/2026 baada ya kukusanya shilingi bilioni 12.1, dhidi ya lengo la shilingi bilioni 10 lililowekwa na Bunge.
Mafanikio hayo yamepatikana huku kukiwa bado na miezi miwili kabla ya kumalizika kwa mwaka wa fedha, hali inayoonesha kuimarika kwa mifumo ya ukusanyaji wa mapato pamoja na usimamizi madhubuti wa rasilimali za halmashauri hiyo.
Akizungumza katika kikao cha robo ya tatu cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga, Mkuu wa wilaya ya Mbinga Mhe. Kisare Makori, amesema hatua hiyo ni matokeo ya ushirikiano mzuri kati ya viongozi, watendaji na wananchi katika kuhakikisha mapato ya ndani yanaongezeka.
Amebainisha kuwa halmashauri imeweka mikakati madhubuti ya kudhibiti upotevu wa mapato, kuboresha vyanzo vilivyopo pamoja na kuibua vyanzo vipya, jambo lililochangia kufikiwa na kuvukwa kwa lengo hilo mapema.
Mhe. Makori ameipongeza halmashauri kwa mafanikio hayo na kuwataka madiwani pamoja na watendaji kuendeleza juhudi hizo ili kuhakikisha maendeleo ya wananchi yanaendelea kuimarika kupitia utekelezaji wa miradi ya kijamii na kiuchumi.


Comments
Post a Comment