WAZIRI KAPINGA AZITAKA HALMASHAURI ZIACHE VIKWAZO KWA VIJANA WANAOHITAJI MIKOPO.
Mazingira ya sasa yanalazimisha kufanya hatua za ziada kwa ajili ya kuwasaidia vijana. Hivyo, halmashauri zimetakiwa kuhakikisha zinawawezesha vijana na siyo kufanya udhibiti katika mikopo ya asilimia 10, ambapo maafisa maendeleo ya jamii wanatakiwa kuwasaidia vijana ili wakidhi vigezo vya kupata mikopo na siyo kuweka pembeni nyaraka zao ambazo hazijakidhi vigezo.
Akiongea na vijana wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga katika uzinduzi wa jukwaa la uwezeshaji wa kiuchumi kwa vijana wa halmashauri hiyo Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe Judith Kapinga, amesema mazingira ya sasa yanalazimisha kufanya hatua za ziada za kuwasaidia vijana kukua kiuchumi, ambapo maafisa maendeleo ya jamii wanatakiwa kuhakikisha wanawasaidia vijana ili waweze kukidhi vigezo vya kupata mikopo na siyo kuweka pembeni nyaraka zao ambazo hazijakidhi vigezo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga, ndugu Joseph Kashushura, amesema halmashauri hiyo imeweka mikakati ya kuwasaidia vijana ili wakidhi vigezo vya kupata mikopo, ambapo halmashauri hiyo tayari imeweza kutoa mikopo ya asilimia 10 yenye thamani ya bilioni 1.2 kwa vikundi mbalimbali vya Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga. Amesisitiza kuwa bado halmashauri hiyo ina fedha za kuendelea kuwakopesha vijana.
Kwa upande wao, vijana wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga wamesema kuwa changamoto kubwa inayowakuta vijana wengi ni kukosa elimu ya fedha, jambo ambalo limewafanya kushindwa kuwekeza katika viwanda vidogo vidogo au katika kilimo. Hivyo, kutokana na kupata semina hiyo, wameahidi kuhakikisha wanabadilika kifikra na kuinuka kiuchumi.
Comments
Post a Comment