DKT. ABBAS AHAMASISHA WAKAZI WA DAR ES SALAAM KUSHIRIKI TAMASHA LA FUNGA MWAKA KIJANJA TALII
Tamasha la Funga Mwaka Kijanja Talii Msimu wa Pili linaloendelea katika Viwanja vya Sabasaba, jijini Dar es Salaam, limeelezwa kuwa fursa adhimu kwa wakazi wa jiji hilo na Watanzania kwa ujumla kushiriki kikamilifu katika utalii wa ndani kwa kujionea vivutio mbalimbali vya wanyamapori.
Tamasha hilo lililoanza mwezi Desemba 2025 na linatarajiwa kufikia tamati Januari 05, 2026, ni sehemu ya kampeni kubwa ya kitaifa ya kuhamasisha utalii wakati wa msimu wa sikukuu na kufunga mwaka. Limeandaliwa na kuratibiwa na Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Bodi ya Utalii Tanzania (TTB).
Akizungumza mapema leo Desemba 24, 2025, wakati wa ziara ya kutembelea tamasha hilo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbas, ametoa wito kwa wakazi wa Mkoa wa Dar es Salaam na mikoa ya jirani kujitokeza kwa wingi kushiriki tamasha hilo ili kupata elimu ya uwekezaji katika sekta ya utalii, kushiriki biashara ya nyara na kupata kitoweo cha nyama pori kwa njia halali, sambamba na kujionea wanyamapori hai wa aina mbalimbali.
“Tunaomba wananchi wa Dar es Salaam na mikoa ya jirani waje katika viwanja vya Sabasaba, Kilwa Road, kujionea wanyamapori hai. Mimi mwenyewe nimejionea simba, duma, tembo na ngiri maarufu ‘Kasongo’, naye yupo hapa,” alisema Dkt. Abbas.
Aidha, Dkt. Abbas amesema sekta ya utalii nchini inaendelea kuwa imara na kuonesha ukuaji mkubwa licha ya changamoto mbalimbali zilizoikumba dunia na taifa kwa ujumla. Amebainisha kuwa kuanzia Januari hadi Novemba 2025, idadi ya watalii imeongezeka kwa asilimia 9 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka 2024.
“Kuanzia Januari hadi Novemba 2025, Tanzania imepata ongezeko la watalii kwa asilimia 9, sawa na watalii laki moja na sabini na tatu elfu (173,000) zaidi ikilinganishwa na mwaka jana,” alisema Dkt. Abbas.
Ameongeza kuwa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) imeendelea kufanya vizuri, ambapo kwa takwimu zao, idadi ya watalii wa nje imeongezeka kwa takribani asilimia 18 huku watalii wa ndani wakiongezeka kwa asilimia 40.
Dkt. Abbas ameeleza kuwa mafanikio hayo yanatokana na jitihada za serikali katika kutangaza utalii, kuboresha miundombinu na kuimarisha usalama katika hifadhi zote nchini, hali iliyochangia kuongezeka kwa watalii wa ndani na wa nje.
Kwa upande wake, Kaimu Kamishna wa Uhifadhi wa TAWA, Mlage Yusuf Kabange, amesema kuanzishwa kwa tamasha hilo kulitokana na maombi ya wananchi waliotamani kupata muda wa kutosha zaidi wa kuwaona wanyamapori, maombi yaliyokuwa yakitolewa wakati wa Maonesho ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba).
“Wakati wa maonesho ya Sabasaba, wananchi wengi walieleza kuwa muda wa kuwaona wanyamapori haukutosha. Tukaamua kuja na mkakati huu wa kuleta wanyamapori wakati wa likizo ili wanafunzi wapate muda wa kutosha, wakisindikizwa na wazazi wao,” alisema Kabange.
Ameongeza kuwa kupitia tamasha hilo, ni kama mbuga zimehamishwa kutoka porini na kuletwa Dar es Salaam, kwa kuwa wanyama waliokuwa hawajawahi kuoneshwa awali, kama tembo, ngiri na aina mbalimbali za swala, wameongezwa ili kukidhi matakwa ya wananchi.
Tamasha la Funga Mwaka Kijanja Talii linaendelea kuwa kivutio kikubwa kwa wakazi wa Dar es Salaam na wageni kutoka maeneo mbalimbali nchini, likilenga kuimarisha utamaduni wa utalii wa ndani na kuongeza uelewa wa jamii kuhusu uhifadhi na matumizi endelevu ya rasilimali za wanyamapori.




Comments
Post a Comment