CUF-ZUIO LA MIKUTANO YA HADHARA KWA VYAMA VYA SIASA NI HARAMU NA HALIKUBALIKI
CUF- Chama Cha Wananchi tumepokea taarifa ya kupigwa marufuku kwa mikutano ya HADHARA kwa Vyama vya Siasa kwa mshangao na masikitiko makubwa.
Kauli iliyotolewa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi kuhusu kuzuia mikutano ya hadhara kwa vyama vya Siasa haikubaliki na kwa vyovyote vile ni kichocheo kingine cha vurugu katika kipindi hiki ambapo bado Taifa linaugulia ya majeraha yaliyotokana na vurugu na Mauaji ya Oktoba 29, 2025.
Mapema mwaka 2024 Dkt Samia Suluhu Hassan akiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kufuatia kifo cha Rais Dkt John Pombe Magufuli aliweka bayana kwamba Mikutano ya hadhara kwa vyama vya Siasa ni Haki ya Kikatiba na Kisheria, hivyo kuizuia haikuwa sawa. Tunamkumbusha Waziri Katambi kwamba kwa vyovyote vile sauti yake haipaswi kupanda juu ya Sauti ya Mteuzi wake na kwamba Katiba na Sheria alizozirejea Dkt Samia Suluhu Hassan mwaka 2024 havijabadilika.
Kupitia mabadiliko ya wakati, CUF- Chama Cha Wananchi kiliitahadharisha Serikali ya Awamu ya tano kutorejea makosa yote yaliyofanywa na Hayati Magufuli katika kukandamiza Demokrasia, Haki za Binadamu na Utawala wa Sheria na tukaonya kwamba mpango wowote wa kuvuruga Uchaguzi Mkuu wa 2025 usingepokelewa kinyonge kama ilivyokuwa mwaka 2020. Sote tunaendelea kuugulia madonda yaliyotokana na kuvurugwa kwa Uchaguzi wa 2025 baada ya Serikali ya CCM kukaidi kupokea nasaha zetu kupitia kinywa cha Mwenyekiti Mstaafu Prof. Ibrahim Haruna Lipumba.
Miezi miwili iliyopita Mwenyekiti wa CUF- Chama Cha Wananchi Mhe. Mirambo Camil Yusuf alipongeza Mapendekezo ya Uponyaji na Maridhiano, kama yalivyoainishwa kwenye Ripoti ya Tume ya kuchunguza matukio ya Oktoba 29, 2025 chini ya Jaji Chande.
Uponyaji na Maridhiano, kwa vyovyote vile, maana yake haiwezi kuwa ni kufumbia macho sababu mbalimbali zilizoainishwa kuwa ni vichocheo vya vurugu, sababu kubwa ikiwa ni kuminywa kwa Haki zinazokamilisha tafsiri ya Demokrasia ya Kweli. Kwa kuzingatia ukweli huu, Waziri Katambi ni kama anarefusha utambi unaowaka ili moto 'ukolee' katika kipindi ambacho BUSARA inapaswa kutuongoza katika Juhudi za kuuzima. Inawezekana kabisa kwamba yeye ni miongoni mwa wanaomkwamisha Dkt Samia Suluhu Hassan katika kujaribu kuwarudisha Watanzania pamoja, baada ya kukiri kwake kwamba kama Taifa tulijikwaa.
Tunamkumbusha pia Waziri Katambi kwamba Jukumu la Jeshi la Polisi kuhusu Mikutano ya hadhara si KUTOA KIBALI, bali kupokea taarifa na kujipanga kwa ajili ya kuulinda mkutano ili kuhakikisha Ulinzi na Usalama.
CUF- Chama Cha Wananchi tunatoa wito kwa Serikali kuacha desturi ya kuziba masikio kama jaribio la kutosikia mayowe ya wanaodai Haki.
Ni muda muafaka sasa kwa Serikali kuyaingiza kwenye Utekelezaji Mapendekezo ya Tume ya Jaji Chande kuhusu uharaka wa Mchakato wa kupatikana kwa Katiba Mpya inayotokana na Maoni ya Wananchi, ambayo imeshauriwa ipatikane si zaidi ya mwaka 2028. Hakuna muarobaini wala njia ya mkato ya kulitibu Taifa, nje ya kuyafanyia kazi madai ya watanzania ambayo yalianza kumwaga damu za wanachama na wafuasi wa CUF- Chama Cha Wananchi robo karne iliyopita(Januari 26 na 27, mwaka 2001). Tanzania inahitaji KATIBA MPYA yenye misingi Thabiti ya Demokrasia na Utawala Bora.
HAKI SAWA NA FURAHA KWA WOTE!
Eng. Mohamed Ngulangwa
Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mahusiano na Umma
CUF- Chama Cha Wananchi
Juni 26, 2026```

Comments
Post a Comment