MAKAMU WA RAIS DKT. NCHIMBI ATEMBELEA MAONESHO YA KIMATAIFA YA NANE NANE - DODOMA
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi ameitaka Tume ya Maendeleo ya Ushirika kuendelea kufanya usimamizi wa vyama vya ushirika na kutoa miongozo ya kitaalamu kwa vyama vyote nchini.
Makamu wa Rais ametoa wito huo, wakati wa Siku Maalum ya Ushirika katika Maonesho ya Kimataifa ya Nane Nane kwa mwaka 2026, yanayofanyika katika Viwanja vya John Malecela, Nzuguni mkoani Dodoma. Amesisitiza Shirika la Ukaguzi na Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (COASCO) kuhakikisha linaendelea kufanya ukaguzi wa mara kwa mara kwa vyama vya ushirika kwa lengo la kuhakikisha nidhamu ya matumizi ya fedha, kuzuia ubadhirifu na kuongeza uwazi katika uendeshaji wa vyama hivyo.
Makamu wa Rais, amesema Ushirika wenye uadilifu ni muhimu sana katika kujenga imani kwa wanachama na kuvutia uwekezaji zaidi. Amesema kuimarika kwa ushirika kunategemea uwajibikaji, uaminifu na uadilifu wa wanachama, viongozi na watendaji wa vyama vya ushirika.
Makamu wa Rais ametoa wito kwa taasisi za umma na binafsi, wadau wa maendeleo na wadau wote kuipa ushirikiano Tume ya Maendeleo ya Ushirika katika kufanisha utekelezaji wa Kampeni ya "Linda Ushirika, Chagua Uadilifu" iliyozinduliwa hivi karibuni, inayolenga kutokomeza vitendo vya kihalifu ndani ya Ushirika.
Vilevile, Makamu wa Rais ameielekeza Wizara ya Kilimo kupitia Tume ya Maendeleo ya Ushirika kuhakikisha ushirika unaendana na Dira ya 2050 inayoelekeza Vyama vya Ushirika kuwa na mwelekeo wa kibiashara na kuwa kichocheo muhimu cha ujenzi wa uchumi wa viwanda na ukuaji jumuishi wa Taifa. Pia amesisitiza umuhimu wa kutoa elimu na hamasa zaidi kwa wananchi wote ili kujiunga na vyama vya ushirika na kufikia lengo la Mpango wa Maendeleo wa miaka mitano la kufikisha vyama vya ushirika 20,540,850 ifikapo 2030/2031.
Makamu wa Rais amesema katika kukuza sekta ya kilimo na kuongeza mchango wake katika uchumi wa Taifa, Serikali imedhamiria kutoa huduma bora kwa wakulima zikiwemo pembejeo na huduma za ugani kwa wakati. Mathalan, katika kuongeza matumizi ya mbolea nchini, Serikali inaendelea kuimarisha upatikanaji na kuhimiza matumizi ya mbolea kupitia Mpango wa ruzuku ili kuongeza tija na uzalishaji.
Katika hatua nyingine, Makamu wa Rais ameshiriki Maadhimisho ya Miaka 10 ya Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI) yaliyofanyika katika Maonesho ya Nane Nane katika Viwanja vya John Malecela mkoani Dodoma.
Katika maadhimisho hayo, Makamu wa Rais ameipongeza Wizara ya Kilimo, Taasisi ya TARI na wadau wote kwa mchango wao mkubwa katika kipindi cha miaka 10 wa kubuni na kusambaza teknolojia na ubunifu unaoendelea kuleta mageuzi katika sekta ya kilimo na kuboresha Maisha ya wakulima nchini.
Aidha Makamu wa Rais, amewataka watafiti wa Taasisi ya TARI kutafsiri Dira ya Taifa 2050 kuwa matokeo yanayoonekana kupitia tafiti na ubunifu unatoa suluhisho kwa changamoto ya sekta ya kilimo kwa kuongeza tija, ushindani na kuongeza thamani ya mazao. Amesema historia inafundisha maendeleo ya ukweli na endelevu yanajengwa kwa kuwekeza katika rasilimali watu kupitia elimu bora, sayansi, teknolojia na ubunifu, hivyo Dira ya Taifa 2050 imeweka utafiti na ubunifu kama sehemu ya nguzo muhimu za kujenga uchumi imara na wenye ushindani.
Maonesho ya Kimataifa ya Nane Nane kwa mwaka 2026 yanafanyika katika kauli mbiu isemayo “Tambua soko, ongeza tija, kutekeleza Dira 2050”








Comments
Post a Comment